Home » » WANAWAKE WATAKIWA KUACHA UTEGEMEZI

WANAWAKE WATAKIWA KUACHA UTEGEMEZI

Na Amon Mtega, Songea
BAADHI ya wanawake wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wametakiwa kuacha utegemezi kutoka kwa waume zao na badala yake wajitume kufanya kazi.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Margareth Chacha, wakati akizungumza katika mkutano uliojadili namna ya uanzishwaji wa tawi la benki hiyo.

Alisema kama akina mama wanataka kuheshimiwa zaidi na waume zao, ni lazima waonyeshe jitihada ya kuchangia kipato ndani ya nyumba kwa kufanya kazi na kuachana na tabia ya kuwa tegemezi kama ilivyozoeleka kwa baadhi ya wanawake.

“Wanawake wenzangu nawaambieni ukiwa unachapa kazi na kusaidia kutoa mchango wa kipato ndani ya nyumba, hakika migogoro ndani ya ndoa zenu huisha, kwa kuwa mwanaume ataona umuhimu ulionao ndani ya familia,” alisema Chacha.

Alisema kwa utafiti uliyofanywa na baadhi ya wataalamu, wamegundua wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi ya kubuni miradi mbalimbali inayoweza kusaidia kuinua maisha ndani ya familia.

Aidha, alisema kuna changamoto wanayokutana nayo ya wanawake wengi nchini kujirudisha nyuma kuwa hawana uwezo wa kufanya kazi ya kuingiza kipato ndani ya familia, kwa kudai hawana pa kupatia mtaji.

Alisema benki hiyo itawahusisha na wanaume kwa lengo la kutojenga ubaguzi ndani ya familia zao, ingawa nembo yake inaonyesha ni ya wanawake.

Alisema ili tawi hilo liweze kufunguliwa, unahitajika mtaji wa Sh milioni 500.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi mkoani Ruvuma, Vestina Ngurusi, alisema kwa sasa wanatoa elimu kwa wanawake hao juu ya uanzishwaji wa benki hiyo na kushughulikia upatikanaji wa jengo na baada ya hapo wataanza kufanya kazi hiyo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa