Home » » MGAWO WA MAJI WAIKUMBA SONGEA

MGAWO WA MAJI WAIKUMBA SONGEA



na Julius Konala, Ruvuma
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa ya Songea (SOUWASA) imetangaza kuwapo mgawo mkali wa maji kati ya Agosti na Novemba mwaka huu kutokana na upungufu wa maji katika vyanzo vya mtiririko vilivyopo milima ya Matogoro mjini hapa.
Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Francis Kapongo, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na akasema kuwa uzalishaji umepungua kutoka meta za ujazo 9,700 hadi kufikia 7,000 kwa siku.
Alisema kutokana na takwimu za vipimo vya maji kwenye mito inatarajiwa maji ghafi yataendelea kupungua na huenda yakapungua zaidi ifikapo Septemba hadi Novemba na kukadiriwa maji hayo kupatikana kwa viwango vya meta za ujazo 5,400 kwa siku, ambayo ni sawa na asilimia 56 ya mahitaji halisi.
''Hali hii imetokana na mvua zilizonyesha mwaka huu kuwa chache, jambo ambalo limesababisha ukame katika vyanzo vinavyotegemewa kutiririsha maji kuelekea kwenye tanki kubwa linalosambaza, kupungua na kupelekea kuwepo kwa mgawo,” alisema Kapongo.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakazi wa Manispaa ya Songea kuwa wavumilivu katika kipindi hicho na kwamba watahakikisha watapata maji kulingana na ratiba ya mgawo na si vinginevyo hadi hapo mabadiliko ya hali ya hewa yatakapotengamaa.
Pamoja na hayo alisema chanzo cha akiba cha Luhira ambacho kilikuwa kinazalisha meta za ujazo 12,800 kimepungua na kufikia uzalishaji wa meta za ujazo 3,200.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa