Home » » MADIWANI RUVUMA WAONYWA

MADIWANI RUVUMA WAONYWA


na Julius Konala, Songea
KATIBU Tawala Mkoa wa Ruvuma (RAS), Hassan Bendeyeko amewataka madiwani katika halmashauri kuacha kuwafukuza kazi watumishi kwa sababu zisizo za msingi.
Bendeyeko alitoa rai hiyo jana mara baada ya kupewa nafasi ya kujitambulisha na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Rajabu Mtiula katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Jumba la Maendeleo mjini Songea.
Alisema kuna baadhi ya watumishi katika halmashauri mbalimbali mkoani Ruvuma wamesimamishwa kazi au kuachishwa baada ya kuadhibiwa na madiwani hao kutokana na sababu zisizohusiana na utendaji kazi wao.
Bendeyeko alisema sababu nyingine inayosababisha kuzorota kwa halmashauri ni kutokana na kukithiri kwa migogoro baina ya madiwani na watumishi katika halmashauri hizo.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa migogoro mingi kati ya wakuu wa idara na madiwani katika halmashauri inatokana na kunyimana fedha za miradi ya maendeleo.
Aidha, katibu tawala huyo wa Mkoa wa Ruvuma aliwataka madiwani hao kuhakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kuondokana na kupata hati chafu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkirikiti aliwataka watumishi na watendaji wa halmashauri hiyo kujenga tabia ya kuwajibika katika maeneo yao ya kazi na kutatua kero za wananchi badala ya kutumia muda mwingi kufunga ofisi na kuzunguka mijini pasipo sababu za misingi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa