na Stephano Mango, Tunduru
WAKAZI wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamehimizwa kutoa ushirikiano katika ulinzi wa maliasili za taifa, ili wananchi wote waweze kufaidi matunda ya rasilimali hizo.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho wakati akifungua mafunzo ya siku 15 kwa wanajumuiya wanaojishughulisha na uhifadhi wa maliasili kwa jamii za jumuiya za hifadhi za Nalika na Chingoli.
Mbali ya kupongeza juhudi za uendeshaji wa mafunzo hayo, alisema kupitia mafunzo hayo serikali inaamini kuwa kila mtu atatimiza wajibu wake na kutokomeza ujangili.
Akizungumzia faida za mafunzo hayo, Mkurugenzi wa mradi wa kuhifadhi ushoroba mtambuka wa Selous – Niassa, Kumrwa Ngomelo, alisema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Wananchi wa Ujerumani – KfW, unalenga kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa rasilimali za maliasili hususani wanyamapori kwa kuunda jumuiya za uhifadhi (Wildlife Management Areas).
Alisema, mafunzo hayo yanalenga kupambana na tatizo la ujangili ambao wananchi pia wamekuwa miongoni mwa washiriki wa vitendo hivyo na kufichiana siri kwa matukio hayo.
Wakizungumzia hali ya ujangili wilayani Tunduru, Ofisa Wanyamapori, Peter Mtani na mshauri Idara ya Maliasili Wilaya ya Tunduru mradi wa Wanyamapori Selous – Niassa, Elias Mungaya, walisema taifa lisipochukua hatua za makusudi kudhibiti uwindaji haramu kupitia uanzishwaji wa jumuiya hizo, ubinafsishaji na uwindishaji wa kitalii hautakuwa na faida yoyote kwa watalii na wawindaji hao.
Akizungumza kwa niaba ya wanajumuiya hao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chingoli, Dauda Mohamedi, alisema baada ya mafunzo hayo, wajumbe hao watatekeleza majukumu yao bila woga tofauti na awali ambapo kulikuwa na tabia za kutupiana majukumu kati ya viongozi wa serikali na jumuiya hizo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment