Home » » MADIWANI WAFUNDWA KUHUSU SENSA

MADIWANI WAFUNDWA KUHUSU SENSA


na Julius Konala, Mbinga
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kushiriki kikamilifu, kuhamasisha wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi katika sensa ya watu na makazi kwa lengo la kuhesabiwa.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Senyi Ngaga, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa madiwani hao, kuhusiana na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 26.
Ngaga alisema madiwani hao wana wajibu mkubwa katika kata zao, kwa kuwaelimisha wananchi kushiriki mchakato huo ambao taifa linategemea kupata takwimu sahihi za idadi ya watu ambazo zitasaidia kupanga shughuli za maendeleo.
Naye Mratibu wa Sensa wilayani Mbinga, Maurus Hyera, alifafanua kuwa katika wilaya hiyo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya zoezi hilo ni 747, kati ya hayo 230 yatatumia dodoso refu na yaliyobaki dodoso fupi.
Aliongeza kuwa, wilaya hiyo itakuwa na wasimamizi 76 ambao watawajibika kusimamia kikamilifu katika kuhakikisha shughuli hiyo inaendeshwa katika hali ya usalama kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa kisheria.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa