Home » » MALAWI, TANZANIA KUKUTANA AGOSTI 20

MALAWI, TANZANIA KUKUTANA AGOSTI 20

na Ratifa Baranyikwa
WAWAKILISHI wa Malawi na Tanzania wamepanga kukutana mjini Mzuzu, nchini Malawi Agosti 20 mwaka huu, kwa ajili ya kujadili juu ya mzozo wa mpaka katika Ziwa Nyasa.
Nchi hizo mbili kwa sasa zimeingia katika mgogoro wa maneno baada ya Malawi hivi karibuni kusema kuwa inamiliki eneo lote la ziwa hilo kwa mujibu wa mikataba ya kikoloni.
Hata hivyo, Tanzania kwa upande wake inadai kuwa mpaka baina yake na Malawi umepita katikati ya ziwa hilo ambalo limekuwa likiitwa Ziwa Nyasa wakati Malawi wao wakiliita ziwa Malawi.
Katika mahojiano yake na gazeti la The Nation la nchini Malawi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa nchi hiyo, Ephraim Mganda Chiume, alisema wakati wakifahamu msimamo wa Tanzania kuhusu suala hilo, pande mbili zitakutana pamoja na mambo mengine zitajadili kwa kina juu ya suala hilo.
“Katika mkutano niliokutana na Waziri mwenzangu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania wiki chache zilizopita, iliamriwa kuwa pande zote mbili zikutane Malawi, mjini Mzuzu kwa haki kabisa kuendelea na majadiliano juu ya mgogoro unaoendelea.
“…Nafahamu kile kilichoafikiwa Dar es Salaam juu ya msimamo unaojulikana wa kuzitaka kampuni za Malawi zinazoendelea na shughuli za kutafiti mafuta na gesi katika Ziwa Malawi kusitisha mara moja hadi pale suala la mgogoro wa mpaka litakapopatiwa ufumbuzi,” alisema waziri huyo.
Pasipo kuzungumzia juu ya lolote linaloendelea kuhusu suala hilo wakati huu ambapo kuna ratiba ya mkutano wa Agosti 20, waziri huyo alisema kuwa msimamo wa serikali ya Malawi utajulikana katika muda muafaka na mfupi ujao na kwamba hebu waipe nafasi diplomasia.
Kauli ya Chiume kwa gazeti la The Nation la nchini Malawi imekuja kwa kile gazeti hilo lilichodai kuwa ni baada ya msimamo wa Tanzania kama ulivyoripotiwa katika vyombo vya habari kwenye mtandao vya www.citizen.co.tz, ippmedia.com na in2eastafrica.net Jumanne wiki hii juu ya kauli ya serikali kuyataka makampuni ya yanayofanya shughuli ya kutafuta mafuta na gesi kuacha mara moja, hadi pale suala la mpaka kati ya nchi hizo mbili utakapotatuliwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, aliliambia Bunge mjini Dodoma kuwa kuanzia Agosti 6 mwaka huu hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufanya shughuli ya kutafiti, au kutafuta mafuta katika ziwa hilo ili kuyapa nafasi majadiliano yanayoendelea ya kutatua mzozo wa mpaka.
Mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi si mgeni, suala hilo liliwahi kuibuliwa miaka ya 1960 na muasisi wa Taifa la Malawi, Rais Hastings Kamuzu Banda ambaye alidai kuwa ziwa hilo na eneo lote la mkoa wa Mbeya ni sehemu ya Malawi.
Kamuzu aliripotiwa kuegemea mkataba wa wakoloni Julai 1, 1890 kati ya Uingereza na Ujerumani ambao unasema mpaka kati ya nchi hizo mbili ni pembezoni mwa pwani ya ziwa.
Kwa upande wake, Membe alisema Tanzania ina ramani ya Waingereza ambao wakati huo waliongoza Tanganyika na Nyasaland (sasa Malawi) ambayo inaonyesha kuwa kulikuwa na makubaliano ya kupitia upya mpaka na kuonyesha kuwa ulikuwa ukipita katikati ya ziwa.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa