Home » » RC RUVUMA AWAONYA WANAOINGIZA PEMBEJEO BANDIA

RC RUVUMA AWAONYA WANAOINGIZA PEMBEJEO BANDIA



Na Amon Mtega, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, amewataka mawakala wanaoingiza pembejeo za kilimo ambazo ni bandia kuacha tabia hiyo, kwa kuwa wanawaumiza wakulima.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi, alipoelezea hatua mbalimbali za maendeleo ya mkoa huo, ikiwamo suala la kilimo na ajira zisizo za kitaalamu kwa wazawa wa mkoa huo.

Alisema pamoja Ruvuma kuwa na rasilimali nyingi za kiuchumi, lakini uchumi wao mkubwa ni kilimo hivyo haistahili kwa baadhi ya mawakala wa pembejeo kuwasambazia wakulima zilizokuwa bandia.

“Kumekuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa pembejeo walizosambaziwa na baadhi ya mawakala zimekuwa bandia kwa kuwa zilishindwa kufanya kazi iliyokusudiwa katika suala la kufanikiwa kwa Kilimo Kwanza ipasavyo.

“Serikali inafanya kila jitihada ya kufanikisha Kilimo Kwanza ili wananchi wake waondokane na tatizo la njaa na ndio maana tumeweza kugawa matrekta kwa ajili ya kilimo kwa mikopo kwa wakulima kwa ajili ya kufanikisha Kilimo Kwanza.

“Eneo lililoongoza kupewa lawama hasa upande wa mbolea ambayo ilikuwa ikichanganywa na chumvi na saruji kwa mbolea zilizokuwa zikielekeana na bidhaa hizo jambo ambalo limewakwamisha wakulima kwa kiasi kikubwa,” alisema Mwambungu.

Alisema kwa sasa Serikali itakapobaini kuna watu wanafanya kazi ya kuwaumiza wakulima haitawafumbia macho.

“Wakulima wa mkoa huu shida yao ni kupata pembejeo inayofaa yenye viwango vya ubora kwa kuwa hawa ni watu wanaojituma katika utendaji wa kazi za kilimo ambazo zinafanya mkoa wetu kuwa na heshima kubwa ndani ya Taifa hili,” alisema Mwambungu.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa