Home » » MUFTI ASISITIZA WAISLAMU WASHIRIKI SENSA

MUFTI ASISITIZA WAISLAMU WASHIRIKI SENSA


Na Amon Mtega, Songea
WAISLAMU nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu zoezi la hesabu ya nyumba na makazi (SENSA), itakayoanza Agosti 26 mwaka huu, kwa kuwa hilo si suala la kidini wala la kisiasa bali ni maendeleo ya kitaifa katika kufanikisha utekelezaji wa maendeleo kwa watu wake.

Wito huo umetolewa jana na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba wakati wa baraza la Eid el-fitr ambalo kitaifa limefanyika Ukumbi wa Sekondari ya Wasichana ya Songea mkoani Ruvuma na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama na serikali pamoja na waumini mbalimbali.

Mufti Simba alisema kuwa, serikali imetangaza suala la sensa ambalo ni la kitaifa, ikiwa na lengo la kupata idadi sahihi ya watu wake, ili kufanikisha maendeleo hivyo ni lazima kujitokeza kuhesabiwa kikamilifu.

“Inashangaza kuona baadhi ya watu wanapita kushinikiza watu wasifanye zoezi hilo wakidai halina maana na kuingiza masuala ya kidini, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu zilizowekwa,’’ alisema.

"Ili maendeleo yaweze kupatikana kwa Watanzania na kupata fursa stahiki, ni lazima kujitokeza kwenye zoezi hili la sensa na kuwapuuza wanaopita na kueneza uwongo na kuweka chuki ambazo hazina sababu.

Aidha katika hatua nyingine aliwataka Waislamu kujenga mshikamano wa kimaendeleo, ili waweze kusonga mbele na kuachana na malumbano ambayo yanakwamisha maendeleo kwa vizazi vijavyo, vinavyowategemea.

"Waislamu tumekuwa nyuma sana katika jambo la kujitoa kimaendeleo, hivyo nawaombeni dumisheni mshikamano kwa kuacha malumbano yasiyo na msingi, ili tufanikishe kusonga mbele kimaendeleo,’’ alisema Mufti Simba.

Naye mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu aliyekuwa mgeni rasmi katika baraza hilo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete alisema kuwa, anazipongeza taasisi zote za kidini kwa kuwahimiza waumini wao kushiriki kikamilifu zoezi la sensa.

Katika hotuba yake, Mwambungu alisema kuwa, serikali inathamini michango inayofanywa na taasisi za kidini, kwa kuwa zinasaidia kuleta maendeleo kwa wananchi wake ambao wote ni Watanzania wanaonufaika na huduma hizo.

Alisema kuwa, sensa haihusiani na dini ya mtu bali lengo kubwa la sensa ni kutaka serikali kupata takwimu za idadi sahihi ambazo zitaiwezesha kupanga mipango sahihi kwa kuzingatia idadi itakayokuwepo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Ruvuma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa